This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-2/

Kutoka Mpingaji hadi Mtetezi: Tafakuri binafsi juu ya faida za mafunzo ya elimu mjumuisho, Kameruni

Louis Mbibeh

Louis ni mwalimu wa sekondari wa masomo ya lugha za Kifaransa na Kiingereza kutoka mkoa wa Kaskazini Magharibi nchini Kameruni, ambaye amekuwa akifundisha kwa zaidi ya miaka sita. Hapa anaelezea uzoefu wake wa kujifunza na kutumia mbinu za elimu mjumuisho. Anaonesha changamoto na nini cha kufanya katika kuinua mwamko na kuwashajiisha wengine wote ambao bado wanapinga utekelezaji wa elimu mjumisho

Mawasiliano ya kwanza
Niligundua ni kiasi gani nilikuwa nikikosa kwa miaka kadhaa pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi ambao walitoka darasani mwangu wakiwa wamejifunza kidogo tu au bila ya kujifunza chochote. Jambo hili lilinipa chamgamoto na ndipo nilipoanza kutafiti kuhusu utekelezaji wa elimu mjumuisho kimataifa na kufikiria namna ya kufanyia marekebisho utekelezaji huo ili uendane na mazingira ya darasani nchini Kameruni. Katika kipindi cha miaka miwili, usomeshaji wangu darasani umekuwa bora kwa kiwango kikubwa. Sasa ninajua kwamba elimu mjumuisho si kwa ajili ya watu wenye ulemavu tu lakini inasaidia kufanya maarifa na kujifunza kupatikana kwa wote. Kwa hivyo basi, nia yangu ni kusonga mbele, si tu kwa mtazamo wa ujumla bali pia kushughulikia juu ya aina maalum za ulemavu pamoja na mbinu za usomeshaji katika madarasa yenye wanafunzi wenye aina hizo za ulemavu.

Changamoto na namna ya kusonga mbele
Utekelezaji wa elimu mjumuisho katika mazingira ambapo hadi 75% ya wafanyakazi hawaelewi chochote kuhusu njia za elimu mjumuisho, haikuwa kazi rahisi hata kidogo.

Baadhi ya changamoto nilizokabiliana nazo ni pamoja na:

  1. Mitazamo: wenzangu ambao hawajapata mafunzo kuhusu elimu mjumuisho huwa hawana uhakika kuhusu elimu mjumuisho.
  2. Sera: Kwa vile Kameruni bado haijaandaa sera ya elimu mjumuisho, mara nyingi huwa ni changamoto kuwashawishi watendaji kuhusu thamani ya maswala yanayohusiana na mjumuisho.
  3. Miundombinu: mahitaji ya msingi yanakosekana kwa wanafunzi wote; mfano mteremko wa kushukia au kupandia (ramp), viwanja vya michezo, vifaa vya kujifunzia/ kufundishia, n.k
  4. Mtaala: unalenga zaidi katika kujibu mitihani na ufundishaji wenye mafanikio hupimwa kwa misingi ya ukamilishaji wa programu yote.

Hatuhitaji miujiza katika kutatua changamoto hizi. Mitazamo na sera haviwezi kubadilika kwa siku moja. Kwa hivyo, tunajitahidi kidogo kidogo kuwaeleza wenzetu na kuwafahamisha kuhusu faida za elimu mjumuisho kwa wanafunzi wote. Iwapo walimu wataanza kufundisha kwa mbinu za elimu mjumuisho, bila shaka sera itafuata. Na hii itapelekea kuwa na miundombinu na njia bora zaidi za kujifunzia na kufundishia.

Kozi zitolewazo kwa walimu katika mafunzo ya kila mwaka kupitia programu ya SEEPD ni mpango mzuri unaofaa kupongezwa katika juhudi za kuongeza mwamko kuhusu elimu mjumuisho. Tunaiunga mkono programu hiyo pamoja na washirika wake (CBM, USAID, n.k) na kuwashajiisha kuendelea na juhudi hizo. Kwa maoni yangu Programu ya SEEPD ni moja kati ya njia mwafaka za utekelezaji wa elimu mjumuisho nchini Kameruni.

Naamini faida za mafunzo niliyoyapata tayari zimeanza kujitokeza. Hatuzioni changamoto zilizopo kuwa ni vikwazo, bali ni fursa ya kuweza kuendelea zaidi. Wengi miongoni mwa wafanyakazi wenzangu sasa hivi wamehamasika na kukubali umuhimu wa elimu mjumuisho. Pia wamekuwa na shauku ya kutaka kupata mafunzo zaidi. Naamini huu ni ushahidi wa wazi kuwa kutoa mafunzo kwa walimu zaidi ni jawabu mwafaka.

Louis Mbibeh, c/o The SEEPD Program
Cameroon Baptist Convention Health Services
Nkwen, Bamenda, North West Region, Cameroon
Barua pepe: mbibeh16@yahoo.com