This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-7/

Walimu wa muda wanavysaidia elimu mjumuisho, Togo

Virginie Hallet

Kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita, Togo imekuwa ikitilia mkazo sana katika kuitikia tamko la Elimu kwa Wote. Mpango wa Elimu wa nchi hiyo (2010-2020) ulifanya elimu kwa watoto wenye umri kati ya miaka 5 hadi 15 kuwa ni ya lazima na tangu 2008/9 elimu ya msingi imekuwa bila ya malipo. Kufuatia mpango huo, uandikishaji uliongezeka kutoka 71% mwaka 2006/7 hadi 87% mwaka 2009/10. Hata hivyo, kumekuwa na ongezeko la idadi ya wanafunzi wanaoacha shule pia, jambo ambalo haliwezi kudharauliwa. Katika makala haya, Virginie anaangalia matumizi ya walimu wa muda kama njia ya kuwasaidia kukidhi mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu, ikiwa ni miongoni mwa njia za kupunguza utoro au kuacha shule na kuongeza hali ya ushiriki wa wanafunzi nchini Togo.

Kuongeza ubora kwa ujumla
Kwa ujumla, kiwango cha ubora wa ufundishaji kiko chini sana nchini Togo, na kurekebisha hali hii itakuwa ni hatua muhimu katika kuongeza uwezo wa wanafunzi kupata elimu pamoja na kuongeza ushiriki wao. Mnamo mwaka 2012, Taasisi ya Mafunzo ya Ualimu ilifunguliwa tena baada ya kufungwa kwa miaka 10 kutokana na vurugu za kisiasa. Sasa, walimu wanaweza kupata kozi ya kina kwa muda wa miezi sita kabla ya kuanza kazi, na sio kuanza kufundisha bila ya kuwa na mafunzo yoyote.Kozi hii ni pamoja na mafunzo ya siku tano juu ya elimu mjumuisho. Inatarajiwa kwamba kwa kiasi kikubwa, mafunzo haya yataongeza ubora wa elimu nchini Togo.

Kuanzisha mfumo wa walimu wa muda
Kuanzisha mfumo wa walimu wa muda, hasa mpango wa ubunifu kwa ajili ya walimu wa muda ulianzishwa mwaka 2010, awali katika mji wa Dapaong, Kaskazini mwa Togo. Lengo lilikuwa ni kuweza kushughulikia vizuri zaidi mahitaji binafsi na maalum kwa wanafunzi wenye ulemavu na walimu wao. Awali, walimu watatu wa elimu ya kawaida waliajiriwa, mmoja tu kati yao alikuwa na uzoefu wa kufundisha watoto wenye ulemavu wa kuona. Maandalizi yao kuwa walimu wa muda yalihusisha wiki moja ya mafunzo ya kina ikiwa ni pamoja na Braille, lugha ya alama na mbinu za kutumia wakati wa kuwafundisha watoto wenye aina mbalimbali za ulemavu, ikifuatiwa na ukaguzi wa kila wiki kwa ajili ya ufuatiliaji, pamoja na vipindi vya mafunzo ya kina wakati shule zinapofungwa. Pia, kulikuwa na utaratibu wa kutembelea shule maalum na kufanya kazi pamoja na walimu waliosomea elimu maalum. Kila mwalimu wa muda huzitembelea shule zake alizopangiwa, na huwasaidia watoto kadhaa wenye ulemavu katika madarasa ya kawaida. Jukumu lao kuu ni kuwasaidia watoto hao wakati wa masomo, na kujadili matatizo yoyote ambayo mtoto anaweza kuwa nayo kuhusiana na mwalimu wao.

Kumekuwa na maoni mazuri kutoka kwa watoto wenye ulemavu ambao hufurahia kupata uangalizi wa ziada, na pia kutoka kwa wenzao wasio na ulemavu ambao hufurahia, kwa mfano, kujifunza kutumia lugha ya alama wakati walimu hao wanapokuwa katika makundi madogo madogo na kuwashirikisha na wao pia.

Uhusiano kati ya walimu wa kawaida na walimu wa muda
Walimu wa kawaida nchini Togo kwa ujumla wako tayari kuwakubali watoto wenye ulemavu katika madarasa yao yenye wanafunzi wengi, na kwa kawaida wanakuwa na mtazamo wa kuwakaribisha vizuri.

Hata hivyo, awali walikuwa na wasiwasi kuwa walimu hao wa muda wanaweza kuwa ni wakaguzi. Kwa kipindi cha miaka mitatu sasa, hata hivyo, walimu kwa ujumla wameelewa na wanawaheshimu walimu hao wa muda, na sasa wanawashukuru kwa msaada na ujuzi wao.

Mjini Dapaong, ambapo mpango huo ulianza, bado ni changamoto kwa walimu hao wa muda kutoa mchango katika utayarishaji wa mitaala na mabadiliko ya kimuundo kuelekea katika mjumuisho katika mashule. Hata hivyo, katika eneo la pili kijiografia ambapo mfumo huu unatekelezwa, Kara, kumekuwa na mafanikio mengi zaidi kwa ujumla yanayohusiana na mabadiliko ya kimuundo na utekelezaji wa mipango ya pamoja na ushirikiano kati ya walimu wa kawaida na walimu wa muda. Kikosi cha Handicap International kilipitia mambo muhimu ya kujifunza yaliyojitokeza katika mradi wa awali, na kuanzisha mradi wa Kara ambao ulitia mkazo zaidi juu ya kufanya kazi kwa pamoja tokea mwanzo kabisa.

Leopold ni mwalimu wa muda kwa watoto wenye ulemavu wa kusikia. Anaunga mkono watoto kutumia lugha ya alama wakati wa masomo na anashauri matumizi ya vifaa vya kufundishia kulingana na hali za wanafunzi. Pia, yeye huwaonesha walimu jinsi ya kutumia picha kuwasaidia watoto kuwasiliana na kuelewa kwa urahisi zaidi. Yeye anafanya kazi na watoto wadogo ambao ni viziwi na pia wenzao, huku akiwasaidia watoto wote kujifunza lugha ya alama, kwa kutumia vitendo mbalimbali vya kufurahisha.

Athari
Hivi sasa watoto 54 kati ya 438 wenye ulemavu waliojiunga na shule za kawaida katika maeneo yanayoteuliwa kufanyiwa kazi, wanasaidiwa na walimu wa muda. Hawa ni watoto wanaoishi katika mazingira magumu, na ndio wanaoaminika kuwa ni wenye kuhitaji msaada.

Kwa ujumla, mfumo huu wa walimu wa muda umekuwa na mafanikio. Ni vigumu kutambua kiwango cha maendeleo kwa kuwa mradi ulilenga watoto ambao walikuwa ndio kwanza wameanza shule, hivyo hakuna taarifa za msingi kuhusu kiwango cha elimu cha watoto hao kabla ya kuanza kwa mradi huo.

Hata hivyo, baada ya miaka mitatu ya majaribio, ni dhahiri kwamba watoto wanaosaidiwa na walimu wa muda (wa kupita pita) wanapata mafanikio zaidi darasani kuliko watoto wenye ulemavu ambao hawapati msaada huo, hususan wale walio na ulemavu wa kuona au kusikia. Walimu wa kawaida na familia za watoto hao wameona maendeleo ya stadi za kijamii, mwingiliano na watoto wenzao, na pia stadi za maisha ya kila siku, hata kwa watoto ambao hawajawa na mafanikio makubwa kimasomo. Mfumo wa kutumia walimu wa muda una faida nyingi kwa maisha ya watoto wenye ulemavu pamoja na familia zao nchini Togo.

Video (kwa Kifaransa) kuhusu programu ya walimu wa muda Togo inapatikana kupitia:
www.youtube.com/watch?v=RLlTmUsDBlg

Wasiliana na:
Virginie Hallet
Mratibu wa maradi- Ushirikishwaji na Haki
Mpango wa Handicap International Togo-BENIN
BP 8621 Lomé, Togo.
Barua pepe: coordoinclusion@handicap-international-togo.org

Photos © Sandra Boisseau, 2010, HI