Walimu kwa Wote: Ufundishaji -jumuishi kwa Watoto wenye Ulemavu
Ingrid Lewis
Nchi nyingi hazina walimu wa kutosha waliotayarishwa na kuhamasika vizuri. Hali hii huathiri uandikishaji, ushiriki na mafanikio ya watoto wote, lakini hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa elimu ya watoto walio katika makundi yaliyotengwa. Mara nyingi walimu wanakosa mafunzo au msaada katika kufundisha watoto wenye ulemavu. Hapa, Ingrid anaeleza kwa ufupi njia muhimu zinazoweza kutumika kuandaa walimu wa elimu ya kawaida kwa madarasa yenye wanafunzi mbalimbali.
Viwango vya kitaifa kwa ajili ya mafunzo ya ualimu vinatofautiana kati ya nchi na nchi, na mara nyingi mafunzo hayo huwa duni. Mafunzo ya Ualimu kwa walimu wa kawaida mara chache hujenga kujiamini, maarifa na stadi mbali mbali ili kuwasaidia wanafunzi wenye ulemavu. Utafiti wa hivi karibuni umeonesha mikakati muhimu mitano ya kurekebisha hali hiyo. Kila nchi huweka mkazo tofauti katika maeneo hayo kuendana na mazingira ya nchi hiyo.
1. Watunga sera na wakufunzi wa walimu wanahitaji kuelewa vyema elimu mjumuisho
Wale wanaotunga na kutekeleza sera katika maswala ya elimu na mafunzo ya ualimu wanahitaji ufahamu mkubwa wa elimu mjumuisho ili waweze kukuza ushirikishwaji katika maswala yote ya kazi ya elimu.
Watunga sera na wakufunzi wa walimu wana haja ya:
- kuelewa kwamba elimu mjumuisho si mpango tofauti au ulio mbali (na mfumo mzima wa elimu)
- kuelewa mbinu ya ufuatiliaji sambamba katika elimu mjumuisho, na kuandaa walimu wa kuwasaidia wanafunzi wote kwa ujumla; na kuwa na ujuzi na kuweza kujiamini katika kushughulikia mahitaji ya wanafunzi wenye ulemavu.
- kuelewa umuhimu wa mbinu ya sekta anwai: Ujumuishaji wa watoto katika elimu mara nyingi unahitaji ushirikiano na taasisi mbali mbali kama za kiafya, kijamii -ustawi wa jamii, maji na usafi wa mazingira, usafiri wa umma na sekta zinazohusiana na haki.
Ili kufikia kiwango cha uelewa kinachohitajika miongoni mwa watunga sera na wakufunzi wa walimu, utetezi na jitihada za uelimishaji zinapaswa kuwasilisha ujumbe wa wazi na thabiti juu ya nukta zilizo hapo juu. Kuna haja ya kuwa na mafunzo ya ufuatiliaji na msaada (ikiwa ni pamoja na kuzitembelea mara kwa mara shule pamoja na kukagua miradi ya elimu mjumuisho) ili watunga sera na wakufunzi waendelee kujifunza na kuendelea kuimarisha mafunzo ya kabla ya kazi na mafunzo ya ndani ya kazi yaliyotayarishwa kwa ajili ya walimu.
2. Elimu mjumuisho ni lazima iingizwe katika mafunzo yote ya ualimu.
Elimu mjumuisho inahusika katika nyanja zote za elimu, hivyo kila mwalimu anapaswa kujifunza jinsi ya kufanya elimu iwe jumuishi zaidi. Hii ina maana ya kujifunza jinsi ya kuimarisha mahudhurio ya wanafunzi, ushiriki na mafanikio ya wanafunzi wote, na hasa jinsi ya kusaidia ushirikishwaji wa wanafunzi wenye ulemavu.
Walimu wanahitaji kukubaliana na elimu mjumuisho tokea siku ya kwanza ya mafunzo yao ya ualimu, ili ionekane kuwa ni jambo muhimu kwa kazi yao ya ualimu. Walimu waliopo kazini pia wanahitajika kushiriki katika programu za kukuza maendeleo yao ya kitaalamu ili kuwasaidia waweze mara kwa mara kutafakari na kuifanya mitazamo yao na mazoea yao kuwa bora zaidi. Kuimarisha maendeleo ya kitaalamu inaweza kuwa ni pamoja na mafunzo rasmi wakiwa kazini na fursa za kusoma zisizo rasmi kama vile mbinu za kufanya utafiti katika fani na maeneo ya kazi, na makundi ya majadiliano ya walimu. Kozi kadhaa tu za elimu mjumuisho zisizo na mtiririko maalum hazitoshelezi.
Hatua muhimu zinazohitajika ni pamoja na:
- Kushughulikia elimu mjumuisho katika ngazi zote za mafunzo ya kabla ya kuingia kazini na mafunzo kazini na pia katika programu za kujiendeleza kitaalamu.
- Kutoa mchanganyiko wa (i) kozi maalum juu ya elimu mjumuisho, na (ii) namna ya kuingiza kanuni za elimu mjumuisho katika shughuli zote mafunzo ya ualimu.
- Kupitia na kurekebisha kozi za mafunzo ya ualimu, mitaala na vifaa, na ushiriki kutoka kwa wadau mbalimbali wa elimu.
- Kutetea vyuo vya Ualimu na mawizara kufanya mabadiliko hayo.
3. Mafunzo ya Ualimu ni lazima yawe na uwiano wa nadharia na vitendo.
Mafunzo ya ualimu yanahitaji kuwa na uwiano wa kujifunza kuhusu dhana ya elimu mjumuisho, kuangalia na kutekeleza nadharia hizi kivitendo huku wakisaidiwa na wenzao wenye uzoefu zaidi. Mafunzo ya elimu yanahitaji kuendana na mazingira na utamaduni, kupangwa vizuri ili wanaopatiwa mafunzo ama wasioajiriwa au walimu walio kazini wasijihisi wameelemewa. Mgawanyo wa nadharia na vitendo ni lazima uelekezwe katika changamoto za maisha halisi katika shule katika kuwapatia walimu mafunzo pamoja na stadi zitakazowawezesha kuwa na tafakuri na uchambuzi juu ya kazi yao.
Mambo ambayo yanaweza kuongezewa katika mafunzo ya ualimu kuhusu uzoefu maalum wa vitendo juu ya ulemavu ni pamoja na:
- Kuzishirikisha Disabled People’s Organisations (DPOs) Jumuia za watu wenye ulemavu, watu wenye ulemavu na wazazi wa watoto wenye ulemavu katika kupanga na kuendesha mafunzo hayo.
- Shule maalum mara nyingi zinaweza kutoa msaada wa kiufundi na kiushauri. Hata hivyo, walimu wa shule maalum nao pia wanaweza kuhitaji mafunzo juu ya namna ya kusaidia elimu mjumuisho katika shule za kawaida.
Utaratibu wa mafunzo yanayotolewa kwa awamu unaonekana kuwa na ufanisi kifedha katika kufikisha ujumbe unaokusudiwa kutoka kundi moja hadi jingine. Lakini mara nyingi hausaidii wanafunzi kupata kujifunza kivitendo au kubadilishana mawazo, na ni nadra kuwa na ufuatiliaji wa kutosha. Mitazamo hiyo inahitaji kuimarishwa ili kusaidia shule nzima, kujifunza kutoka walimu wazoefu zaidi, kujifunza kutoka kwa wengine walio rika moja, na ufuatiliaji wa kawaida.
4. Watu wenye ulemavu washirikishwe katika mafunzo ya Ualimu
Kumekuwa na ongezeko la vuguvugu la kutaka ushirikishwaji mkubwa zaidi wa jamii katika uendeshaji wa shule na maendeleo. Ili ifanikiwe, shule ni lazima ishirikishe makundi tofauti yakiwemo ya watu wenye ulemavu. Lakini wale wanaohusika katika upangaji na uendeshaji wa shule hawana ulemavu, wala uzoefu wa moja kwa moja wa kufanya kazi na watu wenye ulemavu. Kwa kuleta ufanisi na uhalisia katika mjumuisho, wadau mabalimbali, hasa watu wenye ulemavu ni lazima washirikishwe. Mikakati yake ni pamoja na:
- Wizara za Elimu ziwashirikishe watu wenye ulemavu wakati wa majadiliano ya sera kuhusu mafunzo ya Ualimu.
- Ni lazima kuwe na upendeleo maalum katika utoaji wa mafunzo, kuajiri, na kuwasaidia wakufunzi wenye ulemavu.
- Kuwakaribisha wakufunzi na wasemaji kutoka makundi na jumuia za watu wenye ulemavu mbali mbali, katika programu za mafunzo ya ualimu ya kabla ya kuanza kazi na pia programu za mafunzo kazini.
- Wanafunzi katika vyuo vya ualimu na katika mafunzo kazini wapatiwe fursa ya kufanya kazi/kujitolea wakiwa pamoja na watoto au watu wazima wenye ulemavu.
5. Wafundishaji wasiwe wa hali moja tu na lazima wawe wanawakilisha makundi mbali mbali
Katika kufikia mjumuisho kwa watoto wote tunahitaji kuangalia kwa makini ni nani anayekuwa mwalimu. Watoto ambao wanahisi walimu wao hawafanani na hali zao, au hawawafahamu, ni nadra kujishughulisha na kujifunza na badala yake wanaweza kutoroka au kuacha shule kabisa. Kwa hivyo basi, kuwa na walimu wenye jinsia tofauti, wenye ulemavu na wasio na ulemavu, na wanaowakilisha makabila, lugha, na dini mbali mbali kulingana na jamii yao ilivyo, ni muhimu.
Watu wenye ulemavu aghlabu hukumbana na vikwazo kadhaa katika kufikia kiwango cha elimu kinachohitajika ili wawe walimu. Hivyo basi, kuna haja ya kuwa na sera nyumbufu katika kuzingatia sifa za kudahiliwa katika mafunzo ya ualimu na\au kubuni na kufadhili kozi maalum za kusaidia kuinua kiwango cha sifa za wale wanaotarajiwa kuomba kudahiliwa. Kadhalika, kuna haja ya kuwekeza katika na kuongeza ubora wa majengo, vifaa vya kujifunzia na kufundishia katika mafunzo ya ualimu.
Watu wenye ulemavu wanaweza kukumbana na ubaguzi katika kupata kazi, ama wakati wa kuchanganua waombaji, au inaweza kuwa tokea mwanzo kuna marufuku kwa watu wenye ulemavu kuwa walimu kutokana na uchunguzi mkali wa kiafya na umakini. Pia kuna uwezekano mkubwa wa kubaguliwa kazini na wenzao au wazazi, au katika muundo wa malipo na fursa za kujiendeleza kitaalamu. Kanuni za uajiri zinahitaji kupitiwa upya na kufanyiwa mabadiliko ili kuondoa vikwazo kama hivyo.
Makala hii inatokana na waraka mkubwa zaidi wa IDDC ulioandikwa na Ingrid Lewis (EENET) na Sunit Bagree (aliyekuwa akifanya kazi Sightsavers zamani), inapatikana katika mtandao: http://bit.ly/1glgWuQ
Contact:
Wasiliana na: Ingrid Lewis, EENET CIC
37 Market Street, Hollingworth
Cheshire, SK14 8NE, UK
ingridlewis@eenet.org.uk