Kusaidia wanafunzi waliotambuliwa kuwa na mahitaji maalum ya kielimu, Moldova
Ludmila Malcoci and Cornelia Cincilei
Katika makala hii, Ludmila na Cornelia wanatusimulia kisa cha Sergiu kuondoka katika taasisi na kwenda katika shule ya kawaida, kwa msaada wa timu ya wataalamu wa fani mbali mbali na kituo cha rasilimali, kama mfano wa kazi kubwa inayofanywa na mradi wa Upatikanaji wa Elimu kwa wote Moldova.
Kisa cha Sergiu
Miaka minne iliyopita, akiwa na umri wa miaka 11, Sergiu alipelekwa shule kwa mara ya kwanza. Jambo hili liliwezekana wakati alipoondoka kituo cha watoto wa kiume wenye ulemavu wa akili Orhei, Moldova, ambako wanalelewa katika familia maalum. Katika hatua hiyo hakuweza kusoma wala kuandika, na alikuwa hawezi kuwasiliana vizuri na watu wengine. Mnamo Septemba 2010, Sergiu alijiunga na darasa la pili katika shule yake ya kawaida, ambapo stadi zake za kijamii, kihisia, na kitaaluma ziliendelea kuimarika. Sasa hivi yuko darasa la sita; akijifunza,na kushiriki katika mazungumzo na shughuli za kijamii pamoja na wanafunzi wenzake. Shuleni, anaendelea vizuri sana, lakini anahitaji msaada katika masomo ya Hisabati, Lugha za Kiromania na Kifaransa. Maendeleo yake hayo ni kutokana na msaada anaoendelea kuupata kutoka kwa walimu wa mjumuisho shuleni pamoja na familia yake ya kambo. Shule anayokwenda Sergiu, ni moja kati ya shule 22 katika Moldova ambazo zimeanza kutekeleza elimu mjumuisho kwa msaada wa Keystone Moldova ikiwa ni sehemu ya mradi wa Equal Access to Education (Upatikanaji sawa wa elimu kwa wote) (EAE). Idara ya Elimu ya Wilaya ya Orhei ilianza mchakato huo mnamo mwezi wa Septemba 2011. Shule anayokwenda Sergiu ilifanyiwa tathmini na timu inayojumuisha wataalamu wa fani mbali mbali ikiwa ni pamoja na Mwalimu mkuu, Msaidizi wa Mwalimu mkuu, walimu, mwanasaikolojia na mtaalamu wa Ustawi wa jamii – ilianzishwa na kuanza kutoa mafunzo. Timu hiyo inashirikiana na familia za watoto waliotambuliwa kuwa na mahitaji maalum ya kielimu, ikiwa ni pamoja na Wazazi wa kambo wa Sergu, ili kuelewa vyema na kuweza kushughulikia mahitaji ya kielimu ya watoto hao. Tangu Januari 2012, msaada wa kielimu anaopata Sergiu umekuwa ukiongozwa na mpango binafsi wa elimu. Mpango huo uliandaliwa na timu ya shule hiyo inayojumuisha wataalamu mbalimbali, wakishirikiana na Keystone Moldova kutoa msaada kwa njia ya mafunzo, usimamizi, ziara za ufuatiliaji na msaada unaoendelea wa kiufundi. Mpango huo unaonesha msaada anaohitaji Sergiu darasani na wakati wa mahudhurio yake katika vikao vya shughuli nyingine zisizo za kitaaluma katika kituo cha rasilimali kwa ajili ya Elimu Mjumuisho kilichoanzishwa na Keystone Moldova, kwa kushirikiana na uongozi wa shule, na viongozi wengine wa serikali katika ngazi za wilaya na jamii. Katika kituo hicho, Sergiu anapata msaada wa kujifunza zaidi, ushauri kuhusu maswala ya kazi, jinsi ya kuzungumza na stadi za kuchanganyika na watu wengine katika jamii. Katika jitihada za kuongeza ufahamu wa jamii juu ya elimu mjumuisho, michezo miwili ya kuigiza inayohusu maswala ya ulemavu – mmoja kwa watu wazima na mwigine kwa ajili ya wanafunzi – ilifanywa na kuigizwa katika kijiji anachoishi Sergiu. Michezo hii imesaidia kuleta mabadiliko ya mtazamo kwa watu wenye ulemavu kutoka kuwaona kuwa ni watu wanaohitaji “huruma na msaada” hadi mtazamo wa kuwaona kuwa ni “watu wenye haki na uwezo [wa kufanya mambo mbali mbali]”. |
Mradi wa Upatikanaji wa Elimu Sawa ni mradi wa miaka minne (ulianza mwaka 2010) unaotekelezwa na Keystone Moldova, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu, jumuia isiyo ya kiserikali ya Step by Step Moldova, na Mamlaka za Umma za Serikali za Mitaa (Local Public Authorities). Msaada wa kifedha unatolewa na Open Society Foundations Early Childhood Programme.
Lengo kuu la Mradi huu ni kusaidia ushirikishwaji wa watoto waliotambuliwa kuwa na mahitaji maalum ya kielimu kwa kushughulikia maswala yote yaani ya kijamii na ya ufundishaji. Mradi huu unatambua upekee wa kila mtoto na ukweli kwamba kila mtoto anakua /anaendelea kwa kasi yake, ana mahitaji ya kipekee ya kielimu, na hujenga ufahamu wake wa dunia yeye mwenyewe.
Mradi unatambua kuwa mtazamo na mabadiliko ya kitabia yanahitajika katika ngazi nyingi. Kwa hivyo Mradi huu unafanya kazi pamoja na wadau wote katika mchakato wa kuandaa mbinu zaidi za elimu mjumuisho, kuanzia katika ngazi ya wizara na kuendelea katika ngazi ya wilaya na jamii hadi katika ngazi ya uongozi wa shule, walimu wa shule, maafisa ustawi wa jamii, washirika wa ndani, wanajamii, wazazi na wanafunzi. Mafunzo na ufuatiliaji kwa walimu wa shule (yanayotolewa na Step by Step Programme) yamesababisha mabadiliko katika mitazamo ya walimu kuhusu mjumuisho wa watoto wenye mahitaji maalum ya kielimu; yamefanya mahusiano ya mwalimu na mtoto kuwa mazuri zaidi;na kwa ujumla, yameongeza ubora wa ufundishaji, kujifunza na mbinu za tathmini.
Hadi sasa, zaidi ya watoto 230 wameingizwa katika madarasa ya kawaida, watu 3,500 (walimu, wazazi, wafanyakazi wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa, wanafunzi, wanajamii n.k) wamepata mafunzo; na vituo vya rasilimali 15 vimeanzishwa katika mashule, kutoa msaada wa ziada kwa zaidi ya watoto 350.
Tathmini ya Faida kwa Walengwa (Beneficiary Impact Assessment) iliyofanywa na Keystone Moldova mwaka wa 2013 ilibaini kuwa mahudhurio miongoni mwa watoto waliotambuliwa kuwa na mahitaji maalum ya kielimu imeongezeka, na pia kiwango cha wazazi wao cha kuridhika na elimu inayotolewa pia kimeongezeka.
“Tuna uhusiano mzuri sana na shule na tumeweza kutatuwa kila tatizo linajitokeza. Tunazingatia kufanya kazi kwa pamoja, na kwa pamoja tunaweza kufanya mambo makubwa. ” Mfanyakazi wa Ustawi wa jamii, Kijiji cha Susleni, Wilaya ya Orhei. |
Tathmini ya Faida kwa Walengwa pia ilibaini kuwa:
- watoto wote waliopata msaada uliokusudiwa walikuwa wakifanya vizuri shuleni.
- Watoto waliotambuliwa kuwa na mahitaji maalumu ya kielimu waliweza kupata marafiki zaidi shuleni, na walizidi kukubaliwa na wanafunzi wenzao.
- Wazazi wa watoto wenye ulemavu walipata taaluma zaidi kuhusu haki za watoto wao na mahitaji na pia walishiriki zaidi katika kusaidia mjumuisho wa kijamii.
- Shule 22 zilizoteuliwa kuwa za majaribio zinatoa mafunzo ya elimu mjumuisho na kutoa msaada kwa shule nyingine za jamii katika wilaya zao.
Mambo ya kujifunza
Mradi huo tayari umebaini mambo kadhaa muhimu ya kujifunza, ikiwa ni pamoja na:
- Utekelezaji wa elimu mjumuisho si mchakato rahisi, unahitaji mashirikiano endelevu ya sekta mbalimbali katika ngazi mbalimbali.
- Uanzishaji wa elimu mjumuisho ni mchakato unaokwenda hatua kwa hatua na unahitaji tathmini binafsi ya kila baada ya muda fulani kutokana na mtazamo wa wanafunzi, wazazi, walimu wasaidizi na wanajamii kwa ujumla.
- kujenga uwezo wa wazazi, watu wenye ulemavu na walimu wa shule katika utetezi kunaweza kuongeza upatikanaji wa elimu bora kwa watu wote. Njia za uelimishaji zisizo rasmi kama michezo ya kuigiza, midahalo, mijadala, ufanyajikazi katika vikundi n.k, zinasaidia sana kupunguza unyanyapaa na ubaguzi.
Wasiliana na:
Ludmila Malcoci, PhD
Mkurugenzi Mtendaji wa Keystone Moldova
Tel: +373 69501709
barua pepe: lmalcoci@keystonehumanservices.org<
Cornelia Cincilei, PhD
Mkurugenzi wa Step by Step Moldova
Simu: +373 69122791
barua pepe: ccincilei@gmail.com