Jukumu la watu wenye ulemavu katika mafunzo ya ualimu, Iraq
Karen Chesterton Khayat
Maendeleo ya elimu mjumuisho lazima yajengwe juu ya msingi wa kushirikisha wadau wote muhimu – watoto, wazazi, walimu, watoa maamuzi, wafadhili, na bila shaka, wawakilishi wa makundi yaliyotengwa. Njia muhimu ya kuhakikisha walimu wanatayarishwa vizuri kuwasaidia watoto wenye ulemavu katika madarasa yao ya kawaida ni kuhakikisha kwamba wanapata uzoefu wa vitendo kwa kufanya kazi pamoja na watoto na watu wazima wenye ulemavu, na kwamba mafunzo wanayoyapata yanaongozwa na mitazamo ya watu wenye ulemavu. Hapa, Karen anaangalia mipango ya kufanikisha haya nchini Iraki.
Kaskazini mwa Iraq (katika majimbo matatu ya Sulaimany, Dohuk na Erbil katika Kurdistan) Wizara ya Elimu ilianzisha mafunzo kwa ajili ya walimu walioajiriwa na Wizara hiyo na pia kuendesha vikao vya uelimishaji kwa viongozi wa elimu. Mafunzo hayo hutoa ‘utangulizi wa elimu mjumuisho’ kwa ajili ya walimu walioko kazini ambao wanataka kusaidia watoto wenye ulemavu katika shule. Mafunzo yalianza kwa kutolewa kozi za mafunzo kwa ajili ya wakufunzi, na sasa kozi zinazotolewa mara kwa mara kwa walimu. Kozi hizi wakati mwingine zinafadhiliwa na UNICEF na wakati mwingine zinafadhiliwa na Wizara.
Katika kozi hizi, watu wazima wenye ulemavu wa kusikia na wenye ulemavu wa kuona wanakuwa pamoja na kusimulianana uzoefu wao na habari zao binafsi za kielimu, jambo ambalo husaidia washiriki wa mafunzo kuelewa nafasi ya elimu katika maisha yao. Wameonesha vifaa saidizi na zana, na pia mbinu zinazotumika katika maisha ya kila siku kwa wanaoishi na ulemavu wa aina moja au zaidi.
Watu wazima ambao ni viziwi wamekuwa wakishirikishwa katika kozi za kufundisha lugha ya alama katika hatua ya awali kwa walimu, kwa kutumia orodha ya maneno ambayo walimu wenyewe wanataka kujifunza, na pia kuonesha namna ya kusimulia hadithi.
Katika semina za uelimishaji kwa walimu wakuu, maafisa wa elimu watoa maamuzi na watu wenye ulemavu wanashirikishwa ili kuleta mitazamo yao kuhusu mjumuisho katika majadiliano wakati wa semina, na kuelezea kwa washiriki wengine uzoefu wao binafsi kuhusu elimu. Wazazi wa watoto wenye ulemavu pia walishiriki katika vikao vya maswali na majibu. Watetezi wa haki za ulemavu wamechangia katika mafunzo hayo kwa kuwa wahadhiri kutoka nje, ili kuelezea kwa kina habari za kinadharia na vitendo, na kutoa ujummbe unaopinga vikali ubaguzi.
Maoni kuhusu kozi hizo yanaonesha kwamba kushiriki na kuchangia vizuri kwa watu wenye ulemavu katika mafunzo hayo kumesaidia walimu kuwaona watu wenye ulemavu kuwa ni washirika katika kuunga mkono haki za watoto katika madarasa yao, badala ya kuwaona kama ni wapokeaji sadaka tu wasio na mchango wowote.
Wachangiaji katika kozi hizo kwa kiasi kikubwa wamekuwa wakipatikana kupitia Jumuia za Watu wenye Ulemavu (DPO’s). Shughuli mbali mbali katika mafunzo hayo zimesaidia kuanzisha au kuimarisha ushirikiano kati ya Jumuia za Watu wenye Ulemavu (DPO’s) na mpango wa Elimu Mjumuisho. Ingawa katika baadhi ya nchi si Jumuia zote za Watu wenye Ulemavu zina uwezo wa kusaidia mafunzo ya walimu, ni muhimu kujifunza kutoka kwao na kujitahidi, ili kuhakikisha kwamba makundi yote mawili,wanajamii kwa ujumla na wataalamu wenye ulemavu wote wana jukumu katika kubuni na kutoa mafunzo juu ya ushirikishaji na usawa.
Walimu viziwi wakiwafanyisha mazoezi
ya lugha ya alama walimu wasio viziwi
Mshauri Mwelekezi aliisaidia Wizara ya Elimu kubuni kozi na kuendesha mafunzo ya awali. Wizara pia iliunda kamati kwa ajili ya semina za uelimishaji. Kamati hiyo iliundwa na wawakilishi wa elimu na wawakilishi wa Jumuiya za watu wenye Ulemavu. Wafanyakazi kutoka DPO’s waliwawakilisha watu wenye ulemavu wa viungo na hisia, na walikuwa ni watu wenye utaalamu katika masuala ya habari / mawasiliano au sanaa. Kamati iliandaa kampeni ya uelimishaji (ambayo pia ilishirikisha sanaa na muziki) na walisaidia sana katika kuzieneza semina hizo katika kanda yote.
Wasiliana na Karen kupitia barua pepe: krchesterton@gmail.com