This article has been published in Enabling Education Review 2
Click here for publication table of content

Reference:

Link: https://www.eenet.org.uk/enabling-education-review/enabling-education-review-2/eer-2-swahili-translation/2-13/

Kuanzisha mbinu za kujifunza na kufundisha zinazomlenga mtoto, Burundi

Elie Sabuwanka

Kuhakikisha kwamba watoto wenye ulemavu wanaweza kushiriki katika elimu mjumuisho katika shule za kawaida hakuhitaji suluhisho kubwa mara zote. Katika makala hii, Elie anaonesha baadhi ya mbinu za kujifunza na kufundishia watoto ambazo zimetumika katika Mradi wa Handicap International, Burundi kwa kusaidia mjumuisho wa watoto wote katika utoaji wa elimu yenye ubora wa juu.

Muktadha 
Burundi imekubaliana na Malengo ya Maendeleo ya Milenia na ina nia nzuri ya Elimu kwa Wote. Tangu 2005, elimu imekuwa moja ya vipaumbele muhimu vya serikali. Ingawa elimu ya msingi si lazima, watoto hawalipi ada ya shule ya msingi. Kwa sababu hiyo, kiwango cha mahudhurio ya shule kimeongezeka kutoka 63.5% mwaka 2000 hadi 134.6% mwaka 2010. Takwimu hii ambayo inawakilisha jumla ya idadi ya watoto waliotarajiwa kujiandikisha kwa mwaka huo, iko juu kutokana na watoto wengi kuchelewa kujiandikisha na / au kurudia madarasa.

Hata hivyo, elimu ya watoto wenye ulemavu imeachwa kwa sekta binafsi (hasa
kwa taasisi za kidini). Watoto wachache wenye ulemavu ambao wanakwenda shule wanakwenda katika vituo maalum ambavyo ni vichache, na havitambuliwi na Wizara ya Elimu.

Mradi wa majaribio wa elimu mjumuisho
Kwa hivyo, Handicap International ilianza mradi wa majaribio wa elimu mjumuisho mwaka wa 2010, kwa kushirikiana na Wizara ya Elimu na shirika la watu wenye ulemavu, UPHB (Union des Personnes Handicapées du Burundi). Mradi huu unatekelezwa katika shule za msingi sita, na kwa kiwango cha chini katika shule nyingine 45 zilizo katika mikoa ya Bujumbura, Mayorship na Gitega.

Mpango huu wa Majaribio unachangia kuinua ubora katika elimu. Mabadiliko yanaonekana katika tabia za walimu na ufahamu wa kazi zao. Kwa ujumla, ofisi ya ukaguzi wa shule inaona mafanikio ya mtaala wa shule kuwa kigezo muhimu zaidi katika kupima kazi ya walimu. Hivyo, walimu wengi wanafikiri sana kuhusu mtaala na mada mbalimbali wanazozifundisha; ni nadra kufikiri kuhusu hali ya watoto ambao watafaidika kutokana na mafundisho yao. Mradi huu wa majaribio unalenga kubadilisha hili.

Mbinu Rahisi lakini zenye Ufanisi
Faida moja kubwa iliyotokana na mradi huu wa majaribio ni kwamba watoto sasa wanaonekana ndio kiini katika mfumo wa elimu. Siku ya usajili, mwalimu mkuu anapata habari nyingi kadiri ya anvyohitaji kuhusu kila mtoto. Wazazi hawana uzoefu wa kuzungumza kuhusu hali ya mtoto wao, hivyo Mwalimu Mkuu hujadili pamoja nao na hivyo mtoto hujifunza zaidi kuhusu uwezo. Ulemavu au matatizo yoyote aliyonayo mtoto yanatajwa ili shule iweze kutoa msaada bora zaidi. Walimu wanashauriwa kujua na kutumia majina ya kila mwanafunzi katika madarasa yao, badala ya kusema ‘Wewe…’ na kunyoosha kidole kwa mtoto, kama walivyokuwa wakifanya siku za nyuma. Hatua hii rahisi ni muhimu sana kwa ajili ya watoto wenye ulemavu ambao kila siku hubaguliwa na kuitwa majina ambayo yanaashiria ulemavu wao. Kila mtoto mwenye ulemavu ana Mpango Binafsi wa Elimu unaofafanua kujifunza kwake na malengo ya ushirikishwaji wake na wenzake kwa mujibu wa uwezo wake. Mpango Binafsi wa Elimu unapendekeza mikakati ya kujifunzia na kufundishia.

Wazazi, walimu na watoto wana kawaida ya kukutana na kutathmini Mipango hiyo na maendeleo ya watoto, na kuweka malengo mapya na mipango ya utekelezaji.

Walimu wanashauriwa kutumia Mpango Binafsi wa Elimu na kufikiria kwanza kuhusu aina ya wanafunzi wao katika madarasa yao: Wakati wa maandalizi ya somo, wakati wa kufundisha, na wakati wa kupanga kwa ajili ya tathmini.

Mbinu ya kujifunza na kufundishia inayomlenga mtoto zaidi imeanzishwa na wanafunzi wote, wenye ulemavu na wasio na ulemavu, wanaifaidika kutokana na mbinu hii.

Mbinu ya aina hii ya ufundishaji inapelekea watoto kuchanganyika na wengine na kujisikia kuthaminiwa na kujumuishwa zaidi.

Wasiliana na:
Elie Sabuwanka
Meneja wa Mradi wa Elimu Mjumuisho
Handicap International Burundi Programme
S.LP: 5219 Mutanga I, Bujumbura, Burundi
Barua pepe: esabuwanka2003@yahoo.fr;
cdpeducation@hif-burundi.org